4 Oktoba 2025 - 21:53
Mwaka mmoja tangu marufuku ya kusali Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq(as); Sera iliyoratibiwa mahsusi kulenga Ibada za Kidini nchin Bahrain

Kwa mujibu wa wachambuzi, kulengwa kwa mimbari ya Sala ya Ijumaa si suala la ndani tu, bali ni ishara ya juhudi za serikali ya Bahrain kudumisha uhusiano wa karibu na Israel - hata kama ni kwa gharama ya kukandamiza sauti za kidini na za wananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Marufuku rasmi ya kuswali Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq (a.s) ulioko eneo la Al-Daraz, Bahrain, sasa imeingia mwaka wa pili. Wanaharakati wamelitaja tukio hili kuwa miongoni mwa mifano ya wazi zaidi ya mateso na ubaguzi wa kidini uliopangwa dhidi ya wananchi wa Bahrain.

Tangu Ijumaa tarehe 4 Oktoba 2024, vikosi vya usalama vya Bahrain vimeizingira eneo hilo, kufunga barabara zinazoelekea msikitini, na kuweka vizuizi vikali vya ukaguzi - ili kuzuia kuswaliwa kwa Sala kubwa zaidi ya Ijumaa ya Waislamu wa Kishia nchini humo.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mlolongo wa maandamano yaliyokuwa yakifanyika kila wiki baada ya Sala ya Ijumaa kuanzia Oktoba 2023 katika eneo la Al-Daraz, yakilenga kuunga mkono Palestina na Lebanon, na kulaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza. Ijumaa ya tarehe 4 Oktoba 2024 - ambayo ilikuwa Ijumaa ya kwanza baada ya kuuawa kwa Sayyid Hassan Nasrallah- ilipangwa kufanyika maandamano makubwa baada ya Sala, lakini mamlaka za Bahrain zikazuia kuswaliwa kwa Sala ya Ijumaa. Sheikh Ali Al-Sadadi, khatibu wa msikiti huo, akatangaza kuwa Sala ya Adhuhuri itaswaliwa kwa utaratibu wa mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo, waumini walioswali walishiriki maandamano ya amani yaliyofuata, ambayo yalivunjwa kwa nguvu na vikosi vya usalama kwa kutumia gesi ya machozi na kemikali zenye sumu.

Marufuku ya Sala ya Ijumaa ilifanyika sambamba na kuzingirwa kwa Msikiti wa Imam Sadiq (a.s) huko Al-Daraz na Msikiti wa Imam Ali (a.s) katika eneo la Saar. Aidha, mamlaka yalipiga marufuku shughuli zote za kuonesha mshikamano na watu wa Gaza na Lebanon.

Kufuatia vizuizi hivyo, idadi ya wanazuoni na makhatibu walikamatwa au kutishwa. Miongoni mwao ni Sheikh Muhammad Sanqour, aliyekamatwa kwa kukosoa mitaala ya elimu inayokaribiana na Israel, na Sheikh Ali Al-Sadadi, aliyelalamikiwa kwa khutba zake za kulaani uhalifu wa Israel huko Gaza na Lebanon. Wanazuoni wengine wa Bahrain kama Sheikh Ali Rahma na Sheikh Fadhil Al-Zaki pia waliitwa mara kwa mara na kupewa vitisho.

Kwa mujibu wa wachambuzi, kulengwa kwa mimbari ya Sala ya Ijumaa si kwa sababu za ndani pekee, bali kunadhihirisha azma ya serikali ya Bahrain kudumisha uhusiano wa karibu na Israel, hata kwa gharama ya kuwakandamiza wananchi wake wa dini.

Kwa takwimu za Kamati ya Masuala ya Wafungwa nchini Bahrain, katika mwezi wa Oktoba 2024 pekee kulikuwa na visa 87 vya kukamatwa kwa sababu ya kuonesha mshikamano na Palestina na Lebanon, au kwa kuwataja mashahidi kama Sayyid Hassan Nasrallah kwa heshima.

Msikiti wa Imam Sadiq (a.s) hapo awali pia ulikuwa umewekewa marufuku ya kuswali Sala ya Ijumaa kuanzia Julai 2016 hadi Mei 2022 — kipindi kirefu zaidi cha kufungwa kwa lazima kwa nyumba ya ibada katika eneo hilo. Wanaharakati wanasema kurudiwa kwa kitendo hiki ni dalili ya sera inayoendelea ya kudhibiti ibada za kidini, kudhoofisha taasisi za kielimu za kidini, na kuwakandamiza viongozi wa kidini. Ni sehemu ya mkakati mpana unaojumuisha kunyang’anya uraia, kukamata kiholela, na kuwatupa uhamishoni kisiasa.

Wanasheria wa Bahrain wanasema kuendelea kwa marufuku hii ni ukiukwaji wa wazi wa Kifungu cha 22 cha Katiba ya Bahrain kinachohakikisha uhuru wa imani na ibada, na pia ni kinyume na wajibu wa kimataifa wa nchi hiyo. Wameitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Manama shinikizo ili kusitisha sera hii, kuondoa mzingiro wa Msikiti wa Imam Sadiq (a.s), na kuruhusu wananchi wake kushiriki ibada zao za kidini kwa uhuru.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha